GENN MEDIA

KANSAS COLLEGE OF NURSING

Jumatatu, 22 Juni 2015

Mkwasa Apawe Mikoba ya Nooij Kuiokoa Timu ya Taifa Stars iliyochoka Kama Mbwa Koko

 

Kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfukuza kazi kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Mart Nooij pamoja na benchi zima la ufundi la Stars baada ya kipigo cha goli 3-0 kutoka kwa Uganda kwenye mchezo wa kutafuta nafasi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Kufuatia kutimuliwa kwa kocha na benchi zima la ufundi la Stars, kitu pekee kinachotakiwa kufanyika ni kumkabidhi kocha mzawa majukumu ya kukinoa kikosi hicho ambacho kwa sasa kimepoteza mwelekeo kutokana na vipigo vya mfululizo

Charles Boniface Mkwasa ni kocha ambaye anauwezo wa kuichukua timu ya Taifa kwa kipindi hiki cha mpito ambacho tunafikiri nini cha kufanya juu ya haya yote ambayo yametokea. Licha ya makocha wengi hapa nchini kuwa na leseni za ukocha za daraja A, Mkwasa ni kocha ambaye yupo kwenye kazi hiyo kwa muda mrefu akifanya kazi tofauti na makocha wengine ambao wana leseni kama yake lakini wameziweka ndani bila ya kuzifanyia kazi.

Mkwasa ambye kwasasa ni kocha msaidizi wa Yanga chini ya Mholanzi Hans van Pluijm, anauelewa mkubwa wa wachezaji wa Tanzania kuanzia namna ya uchezaji wao na mazingira halisi ya soka la bongo kwa mapana yake. Amesha kutana nao kwenye timu mbalimbali wakati timu yake ilipocheza dhidi ya timu hizo kwenye mechi za ligi akiwa kama kocha.

Lakini tunatakiwa tuelewe kwamba, Mkwasa siyo nabii hivyo hawezi kuyabadili haya yanayotokea hii leo kwa siku moja. Anahitaji muda wa kutosha na ushirikiano mkubwa kutoka TFF na wadau wengine wa soka ili kuweza kupata kile ambacho watu wengi wamekuwa wakikitamani lakini mwisho wa yote wamekuwa wakiishia kwenye maumivu.

Tumekuwa na makocha wengi wa kigeni ‘wazungu’ lakini bado hatujafika popote wala hata nusu ya pale tunapopataka, nikisema hivyo sina maana nawabeza makocha wa kigeni waliowahi kuinoa Stars. Ila naangalia kama walifikia malengo ambayo tumekuwa tukitaka kuyaona kwenye soka letu la Tanzania, kama nao wamekuwa wanakuja wanalipwa mamilioni ya fedha lakini bado wameshindwa kutupeleka pale tunapopataka basi sioni ulazima wa wao kuja.

Kumwamini kocha mzawa na kumpa timu sio dhambi wala si ujinga, kama atapata ushirikiano wa kutosha kama wanaopewa makocha wa kizungu naamini mzawa anaweza akatusaidia kuliko hata hawa makocha wa kigeni ambao kila kukicha wanaichukua timu hakuna wanachokifanya mwisho wa siku tunaishia kuwatimu na kuwalipa pesa nyingi wanatokomea na kuiacha timu ikiwa kwenye hali mbaya.

Mwarobaini wa taizo letu sio makocha wa kigeni hapo naomba tuelewane, hata kama tutamchukua Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho, au Pep Guadiola bado tatizo litabaki palepale kwasababu tatizo letu sisi sio kocha. Tatizo linalolitafuna soka la Tanzania ni mfumo wazungu wao wanaita ‘system’, hapa ndipo imelala mizizi ya matatizo yote yanayolitafuna soka la bongo.

Sasa inabidi kuichimbua mizizi hiyo ili siku moja na sisi tufurahie matunda ya soka kama nchi nyingine ndogo za Afrika ambazo zimethubutu lakini sisi kila kukicha bado tunapiga mark time palepale. Mfano mzuri ni Botswana hawa jamaa waliopata umaarufu kwa ngoma ya ‘makhirikhiri’ walishiriki michuano ya AFCON sisi tukiwa watazamaji kwenye TV zetu. Nchi nyingine ni Burkina Faso wale ambao Erasto Nyoni aliwafunga goli wakiwa kwao baada ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, nao pia walifuzu kucheza AFCON sisi tukawa watazamaji tu.

Sasa ifike wakati tujifunze kukubali vyetu, hebu tumpe huyu mzalendo hii timu wakati sisi tukiangalia tunaanzia wapi kuichimba hii mizizi yetu ya mfumo mbovu ambao unalitesa na kuligaragza soka letu kila kukicha. Ninaposema timu apewe Mkwasa sio kwamba nampigia debe la hasha, ila ukiangalia kwa makocha wazalendo waliopo hapa Tanzania wenye leseni kama ya Mkwasa na wanafanya kazi basi utaungana na mimi kuomba timu hii apewe Mkwasa mbali ya kuwa na leseni ya daraja la juu.

Mfano mzuri ni yule kocha wa timu ya wanawake ‘Twiga Stars’ Rogasian Kaijage, ameweza kuivusha na kuipeleka kwenye michuano ya All Africa Game itakayopigwa Congo Brazzaville. Angalia mazingira anayofanyia kazi, wachezaji alionao na ushirikiano anaopewa kwenye ile timu hapo utajua kuwa hata hawa wazalendo wanajua ila basi sisi tuna kasumba ya kuwadharau na kutukuza hao makocha tunaowaamini kuwa watatufikisha tunapotaka.

Kwasasa Stars ipo kwenye wakati mgumu sana hasa wachezaji wake wanaokipiga kwenye timu hiyo, wameshapoteza mechi tano mfululizo na hiyo inawaondolea hali ya kujiamini pindi wawapo uwanjani. Wakishatanguliwa kufungwa wanakata tamaa wakijua yaliyowakuta kwenye mchezo uliopita yanajiudia tena kwenye mchezo ambao wanacheza kwa wakati huo. Ukijumlisha na mashabiki wao kuwazomea hapo ndio mambo yanakuwa magumu kwao kwani wanakuwa wanacheza kwa presha ya kutaka kuwaridhisha mashabiki.

Endapo tutampa timu Mkwasa, basi tumuache afanye kile ambacho anaona ni sawa kwa yeye kukifanya kwa wakati huo. Tusimpe presha kubwa bali tumuamini, tumpe ushirikiano na kuheshimu yale yote atakayokuwa akiyafanya kwenye kikosi hicho akiamini yataleta mafanikio. Kweli tupo kwenye wakati mgumu lakini tunatakiwa kuwa wavumilivu kwenye hili hasa kwa kipindi hiki cha mpito tulichopo wakati huu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni