
MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Kilifi wanamzuilia mwanamume mmoja aliyechimba kaburi katika shamba la familia yake katika eneo la Tezo, licha ya kutokuwepo mtu wa familia hiyo aliyekuwa amefariki.
Alipoulizwa na jamaa zake kilichomfanya achimbe kaburi, Bw Brownson Kahindi Katana, mwenye umri wa miaka 42 aliwaambia wawe na subira na kwamba wangeona wenyewe ni nani angezikwa katika kaburi hilo.
“Si mnaona ni kaburi. Kwa nini mnashangaa? Nyinyi msiniulize maswali mengi. Subirini tu na muone ni nani atakayezikwa katika kaburi hili,” aliwaambia jamaa zake, kwa mujibu wa kakaye mdogo, Bw Peterson Charo Katana.
Siku moja tu baada ya kaburi hilo kumalizika, jamaa huyo ambaye ni baba wa watoto watano alimvamia mamaye na kuanza kumtandika na kumlazimisha atafute hifadhi katika kanisa moja lililoko katika eneo la Tezo.
Kamanda mkuu wa polisi wa Kaunti ya Kilifi anayeondoka Bw James Kithuka aliwaambia wanahabari kwamba jamaa huyo atafikishwa kortini kukabiliwa na mashtaka kadha likiwemo lile la kumshambulia mamaye. Kisha atashtakiwa kwa kosa la kuchimba kaburi ambalo lilimaanisha kwamba alidhamiria kutenda kitendo cha uhalifu.
“Huwezi kuchimba kaburi kisha utulie nyumbani kana kwamba hakuna jambo lolote unalowaza. Hiki ni kitendo cha kihalifu. Jamaa huyu kwa sasa yuko mikononi mwetu akiendelea kuhojiwa ili aeleze zaidi sababu za yeye kuamua kuchimba kaburi. Hiki ni kitendo cha kusikitisha sana,” akasema Bw Kithuka.
Kamanda huyo wa polisi ambaye alikuwa ameandamana na wanahabari kuzuru kuliko na kaburi hilo, alisema kuwa maafisa wa usalama vile vile wanawatafuta jamaa watatu ambao walikodishwa kuchimba kaburi hilo.
“Kwa sasa pia tunawatafuta jamaa hao ambao walikodishwa na huyu bwana kuchimba kaburi hili. Tunaamini kwamba watakuwa na habari muhimu za kueleza kuhusu kile ambacho wanajua kwani jambo kama hili huwa si la kawaida,” akasema.
Kaka mdogo wa mshukiwa aliwaambia maafisa wa usalama katika eneo la tukio kwamba hata familia pia ilishtuka sana baada ya kugundua kwamba mmoja wao alikuwa amechimba kaburi katika sehemu ya shamba lao bila kuwaarifu.
“Hata sisi tulishtuliwa sana na hatua hiyo. Tuliona tu watu wakichimba kaburi pembezoni mwa shamba letu. Tulipowahoji walisema kuwa wametumwa na kaka yetu. Yeye binafsi alipoulizwa sababu ya hatua hiyo, hakusema jambo lolote muhimu ila tu kwamba watu wasubiri waone yule ambaye angezikwa hapo,” akasema Bw Katana.
Mamaye mshukiwa Bi Dama Katana alisema kuwa mwanawe alikuwa mtulivu sana na walishtushwa na kitendo chake cha kubadilika kitabia katika siku za hivi karibuni na zaidi kusikia kwa ghafla kwamba alikuwa amekodisha watu kuchimba kaburi.
“Mume wangu alifariki mwaka wa 1976 na tangu wakati huo wote, nimelea watoto hawa kwa shida na raha. Mwanangu Brownson ni kijana mtulivu sana na hata sasa hivi siwezi kuamini aliyofanya. Inasikitisha sana,” akasema mama huyo aliyeonekana kuwa na majonzi makuu.
Aidha, mama huyo alisema kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa wiki moja iliyopita tangu kaburi hilo lichimbwe nyumbani kwao na kisha mchimbaji kuamua kukaa kimya baada ya kuwaambia wangojee kujua hatima ya kaburi hilo. Alisema mwanawe alimshambulia ndipo akaamua kutafuta hifadhi kanisani.
Mke wa mshukiwa Bi Nema Kahindi ambaye pia alikuwa katika hali ya mshtuko mkubwa alisema kuwa hata yeye alisikia kutoka kwa majirani kwamba mumewe alikuwa akichimba kaburi ingawa hakuwa amemwambia kwamba ana mpango huo.
Alisema kuwa mumewe ambaye husimamia kibanda cha kuuza mboga katika kituo cha biashara cha Tezo alibadilika na kuwa mtu mwenye shughuli nyingi ila hakujua alikuwa akijishughulisha na jambo la kutisha kama hilo.
“Hata mimi nimeshangaa sana. Sikujua kwamba anachimba kaburi. Amekuwa mnyamavu sana na mara nyingi haongei mambo mengi. Ninajaribu kufikiria bila kupata jibu kuhusu hatua yake ya kuamua kuchimba kaburi hili,” mke wa mshukiwa akaeleza.
Jamaa huyo alielezewa na wakazi kuwa mtu mpole sana na ambaye huongea kwa nadra mno kuhusu masuala ya kijamii.
-Swahili Hub
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni