GENN MEDIA

KANSAS COLLEGE OF NURSING

Jumamosi, 26 Julai 2014

WALIMU WA UDAKTARI WA CHUO CHA IMTU WAHOJIWA NA POLISI KUHUSU RUNDO LA VIUNGO VYA BINADAMU.


Kamanda Kova: WATU 8 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutupa viungo vya binadamu vilivyogunduliwa katika eneo la bonde la Mbweni Mpiji ambapo mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo hivyo vilikutwa vikitupwa. Miongoni mwa wanahojiwa ni pamoja na madaktari wa Chuo Kikuu cha Madaktari, International Medical and Tecknological University (IMTU) cha Dar es Salaam ambao wanafundisha na kusimamia chuo hicho. 

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne ya Julai 22, 2014 Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, amesema polisi walipata taarifa za tukio jioni ya Jumatatu Julai 21, 2014 kutoka kwa raia wema na kuwa jopo la wapelelezi wakiongozwa na Mkuu wa polisi mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura, walifika katika tukio hilo siku hiyo saa 1:00 usiku. Amebainisha kuwa, baada ya kuwasili katika eneo la tukio waligungua kuwepo na mifuko ipatayo 85 yenye rangi nye usiku ikiwa na viungo hivyo. Alisema viungo hivyo ni pamoja na vichwa, miguu, mioyo, mapafu, vifua na mifupa ya sehemu mbalimbali za binadamu. “Viungo hivyo havikuwa na uvundo au harufu ya aina yeyote na vilionekana kwamba vimekaushwa na kukakamaa, lakini wananchi walikuja katika eneo la tukio wapatao 1,000 hawakuwa na taarifa sahihi na ndipo viungo vilichukuliwa na polisi na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi,” anasema Kova. Amesema katika tukio hilo pia vimekutwa vifaa vinavyotumika hospitali ikiwemo mipira ya kuvaa mikononi (gloves) mifuko miwili iliyotumika katika tukio hilo, nguo maalum (apron) zipatazo 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu. Aidha, amesema jopo la wapelelezi saba wanaoongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) Jaffari Mohammed, wameanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kusaidiana na daktari wa polisi anayehusika na uchunguzi wa miili ya binadamu ambaye kwa pamoja wanashirikiana na Madaktari wengine kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Viungo vilitumika mara ya mwisho IMTU Katika hatua nyingine amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya Chuo Kikuu cha Madaktari, International Medical and Tecknological University (IMTU), ambacho pia hufanya mafunzo ya udaktari kwa vitendo jijini Dar es Salaam. Amesema polisi wamewakamata na kuwa wanaendelea kuwahoji watu ambao wanasadikiwa kuhusika na tukio hilo ikiwa ni pamoja na madaktari wa IMTU na kuwa Jeshi hilo limemshirikisha Mkemia Mkuu wa Serikali katika uchunguzi zaidi. Kamishna Kova amesema mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi jalada hilo litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kama itagundulika kukiukwa kwa sheria juu ya jambo hilo hatua zaidi zichukuliwe. Gari iliyokamatwa ikiwa na viungo vinavyotoa harufu Kamanda Kova, amesema polisi walitumia mabomu ya machozi kutawanya wananchi waliotaka kuchoma moto Kituo cha Polisi Bunju ‘A’ ili waweze kumuua dereva aliyekamatwa na gari iliyokua na viungo hivyo. “Ilipita gari pale iliyokuwa imebeba vichwa vya kuku na viungo vingine lakini ilikuwa inatoa harufu, baada ya wananchi kusikia harufu ile wakaanza kuifukuzia na pikipiki hadi dereva wa ile gari akakimbilia polisi kwa ajili ya kujiokoa baada ya kuona anafuatiliwa kwa muda mrefu,” alikaririwa na vyombo vya habari Kamanda Kova. Mashuhuda wa tukio Wakiongea na Gennswahili Julai 22, 2014 baadhi ya wananchi waliokuwa wanafanya kazi za kupasua kokoto katika eneo hilo, wamesema Julai 19, 2014 mchana lilitokea gari ndogo iliyowakuta wakiendelea na shughuli hizo na kuwa waliokuwepo ndani yake hawakushuka bali waligeuza gari yao na kuendelea na safari. “Walipofika hapa waligeuza gari bila kushuka hadi jana nilipokuwa nataka kuchukua mfuko mweusi uliokuwa umewekwa pembezoni mwa njia kwa ajili ya kuwekea kokoto ili nibebe kwa urahisi, nikaoana kucha za binadamu zikiwa zimepakwa rangi ndio nikawaita wenzangu tukatoa taarifa Polisi,” alisema shuhuda mmoja wa eneo hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni