Marekani itasaidia kuanzisha Kikosi cha Dharura cha Kulinda Amani cha Afrika, ambayo ni programu inayodhamiriwa kuyajengea uwezo majeshi ya Afrika katika kukabiliana na migogoro na kusaidia ujumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika barani humo, alitangaza Rais Barack Obama wa Marekani siku ya Jumatano (tarehe 6 Agosti).
"Tutaungana na nchi sita ambayo katika miaka ya hivi karibuni yameonesha rikodi nzuri kama walinzi wa amani - Ghana, Senegal, Rwanda, Tanzania, Ethiopia na Uganda," alisema Obama wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ufungaji wa Mkutani wa Kilele wa wa Viongozi wa Afrika na Marekani mjini Washington, DC. "Na tutazialika nchi kando ya Afrika kuungana nasi kwenye jitihada hizi, kwa sababu dunia nzima ina wajibu kwa mafanikio ya ulinzi wa amani barani Afrika."
Kauli ya Ikulu ya Marekani juu ya ahadi hiyo ilisema Marekani itajitolea dola milioni 110 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano kwa ajili ya programu hiyo.
Marekani itashirikiana na nchi sita "kuiendeleza programu ya kikosi cha dharura, kwa kujenga uwezo kwenye maeneo kama vile mafunzo ya kijeshi, ukarabati wa vifaa na matengenezo, msaada wa kitaasisi, na ufanyaji kazi wa pamoja na vikosi vyengine vya kulinda amani barani Afrika," alisema.
"Mataifa washirika barani Afrika yatajitolea kutunza vikosi na vifaa tayari kwa kutumwa haraka na kuelezea dhamira yao kutumwa kama sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika," ilisema.
Obama pia alisema Marekani inashirikiana na Waafrika katika kuanzisha "mtandao wa kutoa onyo na kuchukua hatua haraka" kutambua mizozo inayojitokeza.
Pia alitangaza mipango ya Mradi wa Usimamizi wa Usalama wa pamoja na Ghana, Kenya, Mali, Niger, Nigeria na Tunisia.
Katika mwaka wa kwanza, Marekani itachangia dola milioni 65 kuimarisha uwezo wa sekta ya ulinzi kushughulia vitisho kutoka makundi ya kigaidi yakiwemo Boko Haram, al-Shabaab, al-Qaida Magharibi na Kaskazini mwa Afrika na mengineyo. Mradi huo pia utashughulikia vitisho vyengine vya usalama ikiwemo magendo ya biashara ya wanaadamu, madawa ya kulevya, silaha na ujangili, uharamia, na migogoro ya ndani na ya kieneo.
"Miradi mingi tunayoiendeleza ilibuniwa kuwa ya ushirikiano ili kwamba nchi hizo kwamba kabisa zishughulikie matatizo haya ndani ya mipaka yao au eneo lao," alisema Obama. "Na Marekani haina hamu ya kujitanua na kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Afrika."
-Sabahi