GENN MEDIA

KANSAS COLLEGE OF NURSING

Jumapili, 17 Agosti 2014

WATU WATANO WAFARIKI WAKICHOTA MAFUTA MOLO

Nyanja, Molo
WATU watano walichomeka hadi wakafa usiku wa kuamkia Jumapili baada ya lori la kubeba mafuta kulipuka wakichota mafuta katika eneo la Nyanja, Molo, kwenye barabara ya Nakuru - Eldoret.
Mkasa huo ulitokea muda mfupi tu baada ya wanakijiji karibu 3,000 kuwazidi nguvu maafisa wa polisi waliofika kuwazuia kuchota mafuta hayo.
Wengine saba walipelekwa na Wasamaria wema katika hospitali za Molo, Eldama Ravine na Nakuru wakiwa na majeraha mabaya ya moto mwilini.
Awali, wanakijiji walikimbia mahali hapo na mitungi na ndoo baada ya kupashwa habari kwamba kuna lori la mafuta lililokuwa limeanguka.

Ghafla polisi walifika kuwazuia kuchota mafuta hayo lakini wakazi wakawatimua kwa mawe huku wakiimba 'Haki yetu, haki yetu! Acha tufe tukitafuta utajiri’.
Polisi walikimbilia usalama ndipo wanakijiji wakaanza kuchota mafuta na wengine kuiba nali nyingine kutoka kwa lori hilo.

Ghafla bin vuu, furaha yao iligeuka kilio pale jamaa mmoja alipojaribu kutoa betri ya lori hilo na papo hapo moto mkubwa ukalipuka na kuteketeza watu hao watano.
Kamishna wa Nakuru, Mohamed Birik, alishangaa kwamba wananchi walikaidi amri ya polisi ambao walikuwa wameweka doria hata ikawalazimu kukimbilia usalama.

“Tangu lini watu wakapiga polisi kwa mawe waondoke ili wachote mafuta? Sasa nani atalipia maisha yaliyopotea?” akashangaa Bw Birik.

Alikuwa ameandamana na Naibu Gavana John Ruto na Mkuu wa Polisi wilayani Bernard Kioko.
Kisa hicho kilitokea karibu kilomita 30 kutoka eneo la Sachang’wan, Salgaa, ambako watu 146 walipoteza maisha yao lori la mafuta lilipolipuka na kuwaka moto miaka minne iliyopita.
Bw Ruto alisema serikali yake itaweka mikakati mwafaka kuhamasisha umma umuhimu wa kukaa mbali na sehemu za ajali kwani mafuta ni hatari.

“Tunakumbuka kilichotokea Sachang’wan miaka minne iliyopita na ni jambo la kushangaza kuona watu wakirudia kosa lilo hilo,” akasema.

Kuvua nguo

Bw Peter Rotich, ambaye alinusurika kifo kwa tundu la sindano kwenye kisa cha jana, alisema alilazimika kuvua nguo zake zote ili kuzuia moto kuenea mwilini.
“Nilijiunga na wanakijiji wengine kuchota mafuta lakini nikiwa mita chache kutoka yalipokuwa moto ulilipuka. Nililazimika kuvua nguo zote kisha nikajitupa ndani ya mtaro wa majitaka. Nimechomeka miguuni,” akasema.
Bw Rotich,ambaye alilazwa kwenye wodi ya Hospitali Kuu ya Molo alisema awali alipita hapo na kupata polisi wameweka doria lakini baadaye alirudi na kupata wameondoka na watu walikuwa wakichota mafuta.
Mwanakijiji, Bi Florence Jeruto alisema wanakijiji walikaidi amri ya walinda usalama na kuwarushia mawe na hivyo kuhatarisha maisha yao wenyewe.
Alisema vijana wengi walijiungana na kudai wapewe nafasi ya kuchota mafuta wakidai hiyo ilikuwa bahati yao.

“Hii imekuwa mtindo kwani lori likianguka wanakijiji hupora mali na kisha kutokomea. Hata asubuhi walikuwa wameiba vitu kutoka kwa lori moja la kusafirisha mizigo na hivyo walikuwa na imani kuwa hata mafuta pia ni 'yao’,” akasema.

Chanzo: Swahili Hub

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni