Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uongozi cha Afrika (African Leadership Centre, ALC) yenye Makao Makuu yake Nairobi, Profesa Funmi Olonisakin
Arusha. Sababu za zinazochochea uvunjifu wa amani na usalama katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla zimetajwa kuwa ni pamoja na umaskini uliokithiri, ukosefu wa ajira sambamba na jamii kuwaachia viongozi pekee jukumu hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano na Utatuzi wa migogoro katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Abubakar Zein aliyasema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu chanzo cha machafukona uvunjifu wa amani miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.
“Hakuna amani bila maendeleo na vivyo hivyo kinyume chake huwezi kupata maendeleo bila amani. Ni jukumu la raia wote ndani ya nchi za jumuia hii kuhakikisha vitu hivi viwili vinakwenda sambamba,” alisema Zein.
Awali, Zein aliuambia mkutano wa siku mbili kuhusu usalama katika Ukanda wa Afrika Mashariki unaoendelea mjini hapa kuwa kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa umma katika ujenzi wa amani na usalama, Eala itashirikisha wananchi wa kawaida katika mijadala ya njia sahihi ya kujenga, kulinda na kudumisha amani miongoni mwa nchi wanachama.
Pamoja na wabunge wa Eala mkutano huo pia unahudhuriwa na wawakilishi kutoka Serikali zote za nchi wanachama wa jumuiya hiyo, asasi za kiraia na waandishi wa habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uongozi cha Afrika (African Leadership Centre, ALC) yenye Makao Makuu yake Nairobi, Profesa Funmi Olonisakin aliwataka wasomi na wanazuoni barani Afrika kuhakikisha tafiti na machapisho yao zinajibu changamoto za jamii wanamoishi.
“Waafrika sasa tuanze kuzungumza na kutatua matatizo yetu wenyewe katika mazingira, mila na desturi zetu badala ya kuacha jukumu hilo kwa wengine,” alisema Profesa Olonisakin, raia wa Nigeria.
Mwanazuoni huyo aliwataka raia na viongozi wa nchi za Afrika ambazo nyingi zinasherehekea miaka 50 tangu kupata uhuru kutafakari nini kitatokea kwa bara hilo miaka mingine 50 ijayo na kuweka mikakati ya kukabili changamoto zilizopo na zijazo.
Mtaalamu wa masuala ya amani na usalama kutoka Sekretarieti ya EAC, Leonard Onyonyi alitaja baadhi ya changamoto za kiusalama ndani ya nchi wanachama kuwa ni pamoja na ugaidi, ukosefu wa uhakika wa chakula, ujangili, vitendo vya rushwa na kuzagaa kwa silaha ndogondogo.
Mkutano huo unafikia tamati leo huku wajumbe wa mkutano wakiazimia kuwa na sera ya pamoja kuhusu masuala ya ulinzi na usalama kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki utakaotoa fursa kwa vyombo husika kupeana taarifa za kiintelijensia.
Taarifa hizo zitasaidia kupambana na kudhibiti uhalifu wa makundi yanayovuka mipaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni